Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » MAMA WEMA USIJISAU, WEWE NI MTU MZIMA!MAMA WEMA

MAMA WEMA USIJISAU, WEWE NI MTU MZIMA!MAMA WEMA


HII ni mara ya pili ninaandika kuhusu Miriam Sepetu, mama mzazi wa muigizaji nyota, Wema Sepetu. Bado ninakumbuka vizuri nilichokiandika mara ya kwanza, ilikuwa ni kuhusu tabia yake wakati ule. Alipenda sana kuzungumza na magazeti kuhusu nyenendo za mwanaye katika uhusiano wake wa kimapenzi na Diamond.
Ingawa ni kweli mzazi ana nafasi muhimu katika maisha ya kimapenzi ya mtoto wake, lakini siyo jambo la busara kuingilia kupita kiasi kama yeye alivyokuwa akifanya wakati ule, maana ilikuwa ni kama yeye ndiye mhusika mkuu.
Ninachoshukuru ni kwamba baadaye alijirudi, akaacha kumsakama Diamond, akakubali maisha yao ni yao na sasa vijana wanatumia vizuri fursa waliyonayo katika ulimwengu wao wa mapenzi. Kwa jinsi wanavyokwenda hivi sasa, halitakuwa jambo la ajabu kama wataishia kufunga ndoa, ingawa historia haiongei vizuri kuhusu ndoa za mastaa, hasa wa Kibongo!
Leo ninazungumza naye kwa mara nyingine, nikiwa na imani kuwa kama ilivyotokea awali, atayafanyia kazi nitakayomweleza. Jumapili iliyopita, Wema Sepetu alifanya sherehe ya kumbukumbu yake ya siku ya kuzaliwa, akitimiza umri wa miaka 26, tokea atoke tumboni mwa Miriam.
Sherehe ilifanyika nyumbani kwake binti, Mtaa wa Bwawani, Kijitonyama jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marafiki pamoja na ndugu wa karibu. Kwa mujibu wa waliokuwepo, ilikuwa ni bonge moja la shoo kuwahi kutokea, kwani licha ya msichana huyo kupewa zawadi ya magari mawili, pia watu walikunywa, wakala na kusaza!
Lakini wakati mama alipopewa nafasi ya kuzungumza chochote, kwa namna ya kushangaza, alianza kuzungumza maneno yasiyofaa kutamkwa na mzazi, yakiwemo matusi dhidi ya Kajala Masanja, muigizaji mwingine ambaye siku hizi ni kama paka na panya na Wema.
Wema na Kajala walikuwa ni marafiki wakubwa na kila mmoja anatambua kuhusu hili. Baadaye katika hali ambayo haikutarajiwa, wakakosana na kuleta uhasama mkubwa kati yao.
Mama alitamka matusi ya aibu kwa Kajala. Ni sawa, ana uchungu na mwanaye, lakini hivi ni kweli uchungu huo unaweza kupoteza busara za mama mtu mzima kuzungumza maneno ya ovyo hadharani?
Katika hali ya kawaida, mama yetu huyu alistahili kutumia nafasi ile kutoa ushauri kwa mwanaye kujiweka mbali na mabifu dhidi ya marafiki zake, tena angeweza kumsihi kufikiria kurejesha urafiki wake kwa Kajala, hata kama ni kinafiki!
Lakini leo yeye anashadadia ugomvi wa watoto, hivi hajui hawa vijana wa sasa hawaeleweki? Itakuwaje hawa masistaduu wakirejesha urafiki wao?
Binafsi naamini hakuna rafiki wala adui wa kudumu katika maisha, kitu cha msingi ni kuwa mwangalifu wa kauli wakati wa mgogoro na kutojianika sana kwenye urafiki. Wema na Kajala ni marafiki watarajiwa, hasa kwa sanaa wanayoifanya!
Mama Sepetu ni mwakilishi wa wazazi, sasa anataka baba na mama zetu nao kwenye shughuli zetu watumie nafasi hizo kuwatukana tuliokosana nao sisi katika maisha yetu ya ujana?
Mama hapa amepotoka na nimshauri tu amuombe radhi Kajala. Matusi haya yanasambaa kwa kasi katika mitandao na simu za mikononi. Natambua wanafahamiana vizuri tu kwa sababu aliishi naye kama mwanaye wakati wa urafiki wao na Wema.
Amtafute na ampigie magoti kwa nia njema kabisa. Hawezi kuonekana mjinga kwa sababu moja ya vitu vinavyompa mtu heshima ni uwezo wake wa kutambua makosa na kuwa tayari kukiri. Asipofanya hivi, kwa sababu zozote, atadharaulika, lakini akiomba radhi, ataonekana muungwana. Ni juu yake kuamua anavyotaka tumuone!

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. BONGO STARS LINK - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by Habarizetuleo TEAM
Proudly powered by MAN DUGX