Nina uzoefu kidogo na mambo ya kazi za
ajira maofisini, nimefanya hivi kwa muda mrefu. Wakati flani nilifanya
kazi katika ofisi zilizo katikati ya jiji, kule mitaa ya Posta jijini
Dar es Salaam.
Ofisi nyingi za serikali na watu binafsi
zinapatikana mitaa ile. Kutokana na sababu hiyo, kuna idadi kubwa pia
ya migahawa, hoteli, mama ntilie, pub na kadhalika.
Kuna mambo mawili makubwa yenye
ushawishi mkubwa wa usaliti. Ofa za chakula au vinywaji na usafiri. Kwa
kawaida, wafanyakazi wa ofisi moja hupenda kutoka pamoja wakati wa
chakula cha mchana, wenyewe tunapendelea zaidi kusema lunch!
Kila mmoja ana sehemu yake anayokula
kulingana na kipato chake, wapo wanaokwenda Southern Sun kupata chakula
cha mchana, na wapo wanaowafuata mama ntilie wanaojibanza kwenye
vichochoro vingi vilivyopo mjini.
Huko ndiko tunakokutana na akina dada
waliovalia vizuri na kupendeza, wakitokea katika maofisi mbalimbali,
huwezi kujua yupi ni mhudumu wa chai, yupi ni bosi, wote wanang’ara. Na
hapa ndipo ofa za misosi zinapoanza kushawishi ngono.
Kijana mmoja mwenye kipato kikubwa
ofisini kwake, atavutiwa na msichana mrembo mwenye mshahara wa wastani.
Ili kumsogeza karibu, atalipia chakula cha siku hiyo na kumualika kwa
kesho yake. Kulipiwa chakula ni jambo dogo, lakini lenye thamani kubwa
sana. Si rahisi mtu aliyekulipia chakula kwa nia njema, ukaacha
kumshukuru na hata kumwelekeza unapofanya kazi.
“Mimi nipo pale Oj Traders,” msichana
anaweza kujita mbulisha jina na kusema anapofanyia kazi huku mkaka
akimweleza kuwa yeye ni mhasibu katika ofisi flani. Watakapo
kutana mara ya pili, wataachiana namba za simu.
Baada ya hapo, mkaka atafanya mbwembwe za kuhamahama maeneo ya lunch ili mradi tu mdada wa watu aingie kwenye laini.
Ukimaliza suala la lunch, kuna hii kitu
foleni, hasa kwa wakazi wa Dar es Salaam. Raha ya kufanya kazi katikati
ya jiji inaingia shubiri kadiri jioni inavyozidi kusogea. Kuanzia saa
kumi, ni vurugu katika vituo vya daladala na hasa wakati kama huu ambao
bodaboda zimezuiliwa kuingia mjini.
Wenye magari binafsi ndiyo wakati wao wa
kujidai, ingawa foleni inawakumba wote. Lakini ni afadhali ukiwa kwenye
foleni ndani ya gari dogo, mko wawili kuliko foleni, umeshika bomba
kwenye daladala.
Siyo rahisi kwa mdada kukataa lifti ya
kijana mwenye gari. Na katika foleni ndefu, ni wazi kwamba hadi mwisho
wa safari, watakuwa wameshabadilishana namba. Kwa msichana, kuwa na
uhakika wa usafiri kila siku ni ukombozi.
Tusidanganyane, hakuna msichana ambaye
hatajua kuwa lunch au usafiri anaopewa unahitaji malipo maalum, ambayo
ni penzi. Hali hii haiko Dar tu, bali nchi nzima na pengine duniani
kote.
Mwanamke aliyeajiriwa anakuwa katika
mitihani mikubwa zaidi ya kusaliti ndoa au uhusiano wake, kwa sababu
hata kama haitakuwa kwenye chakula au usafiri, bado watu anaokutana nao
katika utendaji wake, wanaweza kumghasi. Fikiria anakutana na mabosi,
marafiki wa mabosi wake, wafanya biashara, atapona kweli?
Hata hivyo, simaanishi kama tabia hii inawakumba waajiriwa wote, isipokuwa nadhani ni sehemu kubwa wanahusika!
By Mike Tee
0 comments :
Post a Comment